Picture Gallery Send us feedback

NEWS

MUNDUGWAO, HAFSA WATAMBA TUZO ZA KILI MWAKA 2007

MSANII Che Mundugwao akiwa na kundi la Mbega Arts, juzi aling’ara katika Tuzo za Muziki za Kilimanjaro 2006/07, baada ya kuwa msanii pekee aliyeshinda tuzo mbili katika sherehe zilizofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Mbali na Mundugwao, wasanii wengine waliotamba katika tuzo hizo ni pamoja na Hafsa Kazinja, Rehema Chalamila ‘Ray C’, Banana Zorro, Ambwene Yessaya ‘AY’ FM Academia na Msondo Ngoma.

Mundugwao aliibuka mshindi wa Tuzo ya Wimbo Bora wa Asili ya Kitanzania, baada ya wimbo wake wa Makonde kuubwaga ule wa Kila Munu avena Kwao wa Makonde Group na tuzo nyingine ilikuwa ya albamu bora ya asili ya Kitanzania ambayo pia alilishinda kundi hilo la Makonde.

Usiku huo ulishuhudia wasanii Mwasiti Almasi na Q Jay, ambao ni matunda ya kundi la Tanzania House of Talent (THT), wakishinda kwa Mwasiti kutwaa Tuzo ya Msanii Bora anayechipukia na Q Jay akishinda tuzo ya wimbo wa R&’B akiwabwaga wasanii PNC, Joslin, Matonya na kundi la Top Band.

Kinyang’anyiro kilichoonekana kigumu na kisichotabirika kwa wengi ni cha Tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka ambayo ilikuwa inawaniwa na FM Academia (Dunia Kigeugeu), Twanga Chipolopolo (Hujafa hujasifiwa), Violet (Matonya) na Pressure (Hafsa Kazinja akimshirikisha Banana Zorro). Violet ya Matonya ndio ulioshinda tuzo hiyo.

Tuzo ya heshima ambayo hutolewa kwa msanii aliyebobea aliyetoa mchango mkubwa katika kuendeleza muziki wa Tanzania, ilikwenda kwa msanii maarufu, marehemu Morris Nyunyusa ambaye ngoma zake 12 husika kabla ya kuanza kwa taarifa ya habari ya Redio ya Taifa (RTD).

Tuzo ya Wimbo Bora wa Reggae/ Ragga ilikwenda kwa Twenty Percent (20%) wakati ya Wimbo Bora wa Hip Hop ilikwenda kwa msanii wa kundi la ECT, Ambwene Yesaya ‘AY’ kwa wimbo wake, Usijaribu.

Chidi Benzino aliikwaa Tuzo ya Msanii Bora wa Rap, akiwashinda Fid Q, John Makini, Mansul na Rado, huku mkali mwingine aliyejitoa ECT, Mwana FA akishinda Tuzo ya Wimbo Bora wa Kushirikiana, ambao ni ‘Hawajui’ alichomshirikisha Lady Jay Dee. Katika tuzo ya wimbo wa zouk, vibao vya Pressure, Mama Kumbena (Banana), Niambie (Mwasiti) na Wasiwasi wa Mapenzi (Stara Thomas), viliwania tuzo hiyo. Wimbo wa Pressure wa Kazinja/ Zorro ndio ulioshinda.

Shauku iliendelea ukumbini ulipofika wakati wa kujua waimbaji bora wa kike na kiume, ambao tuzo ziliwaangukia Ray C na Banana, aliyekuwa na furaha kubwa kwani juzi ilikuwa siku yake ya kuzaliwa.

Wimbo wa Nameless kutoka Kenya ulishinda tuzo ya wimbo bora wa Afrika Mashariki, wakati mtayarishaji maarufu wa muziki nchini, Master J, aliibuka mtayarishaji bora huku mtayarishaji mwingine, Said Commorien akitwaa tuzo ya mtunzi bora.

Tuzo za Mwandikaji Bora ilikwenda kwa Mzee Yusuph wa Jahazi Modern Taarab, Mtayarishaji Bora wa Video, Visual Lab, Wimbo Bora wa Kiswahili (bendi) ilitwaliwa na Msondo kupitia Maisha Mzunguko, huku FM Academia ikichukua ushindi wa tuzo ya Albamu Bora ya Kiswahili (bendi).

Kwa taarab, Zanzibar Stars ilinyakua Tuzo ya Wimbo Bora wa Taarab kwa wimbo wa Najiamini na wapinzani wao wakubwa, East African Melody kupitia Hamniwezi walibeba Albamu Bora.

 
Habari zaidi