Mtanzania ang'ara Marathon India
MWANARIADHA aliyeanza kujinyakulia umaarufu katika
mbio za nyika nchini, Osward Reveline wa mjini hapa,
ametwaa medali ya fedha katika mashindano ya kimataifa
ya marathon nchini India.
Mwanariadha huyo ambaye ni mtumishi wa Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro, alitwaa medali hiyo baada ya kushika
nafasi ya pili kwenye mashindano hayo yaitwayo Pune
yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Matokeo ya mashindano hayo yaliyotolewa na Pune International
Marathon yameonesha mwanariadha huyo alitumia muda
wa saa 02:19:23, ambapo aliyeongoza ni wa Swedeni,
Said Regragoui, aliyetumia muda wa 02:18:23.
Matokeo hayo ambayo Majira inayo nakala yake yamewataja
walioingia kwenye kumi bora kuwa ni Josephat Ndeti,
Elkanah Machuka, Ambrose Makau, Lezan Kimutai wote
wa Kenya.
Katika mashindano hayo ambayo nchi zaidi ya kumi
zilishiriki, wengine kwenye kumi bora ni Abebe Siyoum,
Gemechu Kabede na Girma Fente wote kutoka Ethiopia
na Ruslan Deulin wa Russia.
Hata hivyo, aliyewahi kuiletea Tanzania medali ya
dhahabu katika mashindano ya Marathon ya Jumuiya ya
Madola nchini Uingereza, Francis Naali alishika nafasi
ya 12.
Katika mashindano hayo yaliyomalizikia Uwanja wa Nehru,
baada ya kuanzia Kandoji Baba Chowk na kuuvuka mara
mbili mto Mutha kabla ya kumalizikia uwanjani hapo,
msichana wa Tanzania, Monica Samira alikuwa wa 12
pia.
Kwa upande wa wasichana katika mbio za nusu marathon
kwenye mashindano hayo ya Pune, ambayo Wakenya walitamba
katika nafasi tatu za juu, ni Hellen Musyoka aliyetumia
saa 01:13:20 na kushika nafasi ya kwanza.
Pia Mkenya, Cathy Mutwa alikuwa wa pili na Pauline
Mutwa alikuwa wa tatu, ambapo wengine kumi bora ni
Helaria Johanes wa Namibia, Jane Muia wa Kenya, Serkalem
Bisset na Gtenesh Urge wa Ethiopia, Madhuri Gurnule
na Preeti Rao wa India na Gittee Karlshoj wa Denmaki.
|