Mtanzania ang'ara Marathon
India
MWANARIADHA aliyeanza kujinyakulia umaarufu katika mbio
za nyika nchini, Osward Reveline wa mjini hapa, ametwaa
medali ya fedha katika mashindano ya kimataifa ya marathon
nchini India.
Mwanariadha huyo ambaye ni mtumishi wa Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro, alitwaa medali hiyo baada ya kushika
nafasi ya pili kwenye mashindano hayo yaitwayo Pune yaliyofanyika
mwishoni mwa mwezi uliopita.
Matokeo ya mashindano hayo yaliyotolewa na Pune International
Marathon yameonesha mwanariadha huyo alitumia muda wa saa
02:19:23, ambapo aliyeongoza ni wa Swedeni, Said Regragoui,
aliyetumia muda wa 02:18:23.
Matokeo hayo ambayo Majira inayo nakala yake yamewataja
walioingia kwenye kumi bora kuwa ni Josephat Ndeti, Elkanah
Machuka, Ambrose Makau, Lezan Kimutai wote wa Kenya.
Katika mashindano hayo ambayo nchi zaidi ya kumi zilishiriki,
wengine kwenye kumi bora ni Abebe Siyoum, Gemechu Kabede
na Girma Fente wote kutoka Ethiopia na Ruslan Deulin wa
Russia.
Hata hivyo, aliyewahi kuiletea Tanzania medali ya dhahabu
katika mashindano ya Marathon ya Jumuiya ya Madola nchini
Uingereza, Francis Naali alishika nafasi ya 12.
Katika mashindano hayo yaliyomalizikia Uwanja wa Nehru,
baada ya kuanzia Kandoji Baba Chowk na kuuvuka mara mbili
mto Mutha kabla ya kumalizikia uwanjani hapo, msichana wa
Tanzania, Monica Samira alikuwa wa 12 pia.
Kwa upande wa wasichana katika mbio za nusu marathon kwenye
mashindano hayo ya Pune, ambayo Wakenya walitamba katika
nafasi tatu za juu, ni Hellen Musyoka aliyetumia saa 01:13:20
na kushika nafasi ya kwanza.
Pia Mkenya, Cathy Mutwa alikuwa wa pili na Pauline Mutwa
alikuwa wa tatu, ambapo wengine kumi bora ni Helaria Johanes
wa Namibia, Jane Muia wa Kenya, Serkalem Bisset na Gtenesh
Urge wa Ethiopia, Madhuri Gurnule na Preeti Rao wa India
na Gittee Karlshoj wa Denmaki.
|