HABARI/NEWS

2012 Kilimanjaro Marathon imezinduliwa

Maadhimisho ya miaka kumi ya Mbio za Kilimanjaro (Kilimanjaro Marathon), yanayotarajiwa kufanyika Februari 26, 2012 kwa ufadhili wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, yamezinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema wadhamini wameamua kuongeza zawadi za washindi katika mbio hizo kwa asilimia 100.

“Hatua hii ina lengo la kuleta hamasa na ari mpya miongoni mwa wanariadha watakaoshiriki,” Bw. Kavishe alisema wakati wa kutangaza rasmi Mbio za Kilimanjaro za mwaka 2012 na Maadhimisho ya 10 ya mbio hizo katika Hoteli ya Southern Sun jijini Dar es Salaam.

Washindi wa kwanza, wa pili na wa tatu wa mbio za Kilometa 42.195 kwa wanariadha wanawake na wanaume, watapewa jumla ya Tsh 22 milioni.
Katika mbio za Kilimanjaro za tisa, zilizofanyika Feburuari 2011, washindi wa kwanza, wa pili na wa tatu wa mbio za Kilometa 42.195 kwa wanariadha wanawake na wanaume, walijinyakulia jumla ya Tsh 12 milioni.

Mshindi wa kwanza katika mbio za wanaume na zile za wanawake atajipatia kitita cha Tsh 6 milioni huku mshindi wa pili akizawadiwa Tsh 3 milioni na yule wa tatu akiondoka nyumbani na Tsh 1.5milioni. Kwa mujibu wa Kavishe, zawadi kwa washindi wa Nusu Marathon nazo zimeongezeka na kwamba jumla ya Tsh 50 milioni zitatolewa kama zawadi kwa washindi katika mbio zote nne (Marathon, Nusu Marathon, Nusu Marathon ya Walemavu na Vodacom 5km Fun Run).

Viwango vya zawadi za mbio za Km 42.195 kwa washindi wa mbio za wanawake na wanaume.

Mshindi wa kwanza 6,000,000/=
Mshindi wa pili 3,000,000/=
Mshindi wa tatu 1,700,000/=

Kuongezeka kwa zawadi pamoja na msaada mkubwa tunaopata katika kuandaa mbio hizi kutoka kwa serikali, Chama cha Riadha Tanzania, wafadhili washiriki na jamii nzima kwa ujumla wake kila mwaka ni imani yangu kuwa tutaweza kuleta washiriki wengi zaidi katika maadhimisho ya miaka kumi,” alisema.

Akizungumzia jinsi ambavyo Mbio za Kilimanjaro zimekua na kuwa miongoni mwa matukio makubwa zaidi ya kimichezo katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati, Kavishe alisema: “Tangu tulipodhamini mbio hizi kwa mara ya kwanza mwaka 2003, tulipata washiriki 750 na hadi kufikia mbio za mwaka 2011, washiriki walifikia 5,000, walioshiriki mbio aina zote zilizogawanyika katika sehemu nne ambazo ni: Kilimanjaro Premium Lager Marathon, Nusu Marathon, Mbio za Walemavu za GAPCO Nusu Marathon, na Mbio za Vodacom 5km Fun Run”.

Miongoni mwa walioshiriki katika uzinduzi wa Mbio za Kilimanjaro za mwaka 2012 na maadhimisho ya kumi ya mbio hizo ni waliokuwa washindi wa kwanza wa mashindano hayo mwaka 2003, Lucian Hombo na Sara Maja huku mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania, Dioniz Malinzi akiwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bwana Malinzi aliwashukuru wadhamini kwa kuongeza zawadi. “Binafsi nimefurahi sana kusikia kwamba katika mbio hizi wadhamini wameamua kuongeza zawadi kwa washindi…jambo hili litatoa changamoto ya aina yake na kuongeza ushindani…..Sisi kama Serikali, tunatambua mchango wenu mkubwa na tutaendelea kuwaunga mkono ili jitihada zenu za kukuza riadha ziendelee kuzaa matunda,” alisema.

Alisema mbio za Kilimanjaro zimekua kichocheo kikubwa katika kutangaza vivutio vya Utalii nchini. Idadi ya washiriki katika Mbio za Kilimanjaro imeongezeka kutoka 750 mwaka 2003 na kufikia washiriki zaidi ya 5000 waliotoka mataifa 35 katika mbio za mwaka 2011.

Mbali ya Kilimanjaro Premium Lager, GAPCO Tanzania na Vodacom Tanzania, wadhamini wengine wa Mbio za Kilimanjaro za mwaka 2012 ni CFAO Motors, Tanga Cement, TanzaniteOne, Keys Hotel, Precision Air, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, Southern Sun Hotel, KK Security na Bodi ya Taifa ya Utalii

Mbio za Kilimanjaro huandaliwa na Kampuni ya Wild Frontiers ya Afrika Kusini na kuratibiwa na Kampuni ya Executive Solutions wakati Chama cha Riadha cha Taifa na kile cha Kilimanjaro husadia kuratibu na kutoa msaada wa kiufundi.