Wawili kushiriki marathon
China
WANARIADHA wawili wa timu ya taifa ya Tanzania jana waliondoka
nchini kwenda China, kushiriki mbio za Standard Chartered
Marathon, zinazotarajiwa kutimua vumbi Jumapili nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu
Msaidizi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Julius Musomi,
alisema kuwa chama chake kimewateua wanariadha hao wawili
- Paul Sumaye na Fabiola William - ili kuiwakilisha nchi
katika mbio hizo.
Musomi alisema kuwa walipata mwaliko wa kushiriki katika
mashindano hayo kutoka benki hiyo, ambao ndiyo wadhamini
wakuu wa mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa mbalimbali
duniani.
Naye Meneja Uhusiano wa benki hiyo, Joanitha Mramba, akizungumza
katika hafla ya kuwakabidhi bendera ya taifa wanariadha
hao, aliwatakia kila la heri na kuwa wanaamini wataipeperusha
vema bendera ya Tanzania na kurejea na ushindi.
Mramba alisema kuwa mbali na kuwatakia mafanikio wachezaji
hao, pia benki yake imetoa vifaa mbalimbali watakavyotumia
wanariadha hao na gharama mbalimbali za mashindano hayo.
Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni tiketi za kwenda
na kurudi kwa wachezaji, suti za michezo, fulana, kofia,
gharama za chakula, malazi na mahitaji mengine yatakayojitokeza
katika mashindano hayo.
|